Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Kampuni ya Mbolea Tanzania

MBOLEA YA UREA KUANZA KUZALISHWA NCHINI

Imewekwa: 20 May, 2025
MBOLEA YA UREA KUANZA KUZALISHWA NCHINI

 

Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara Bw. Lameck Borega ameshiriki katika hafla ya utiaji saini wa Makubaliano ya awali ya mauziano ya Gesi kwaajili ya kutengeneza mbolea aina ya UREA

Mkataba huo uliosainiwa leo tarehe 19.05.2025 baina ya Kampuni ya ESSA ya Indonesia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni hatua muhimu ya kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha mbolea aina ya UREA, kitakachojengwa Mkoani Mtwara ambapo Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itakua mnunuaji mkuu na msambazaji wa mbolea hii.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara, kwa niaba ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) amepongeza hatua hiyo muhimu na amesisitiza kuwa TFC iko tayari kushirikiana na kampuni ya ESSA ili kuleta urahisi wa upatikanaji wa mbolea hiyo kwa wakulima nchini.

Ameongeza kuwa hatua hii ya uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi, itaokoa fedha za usafirishaji wa mbolea kutoka nchi za nje, itarahisisha upatikanaji wa mbolea kwa haraka na kwa bei nafuu hivyo kumpa mkulima uhakika wa kilimo wakati wote wa msimu.

Kiwanda hicho chenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 1.4, kinatarajiwa kuzalisha zaidi ya tani milioni moja za mbolea kwa mwaka. Kati ya hiyo, asilimia 60 itauzwa ndani ya nchi, huku asilimia 40 ikiuzwa kwenye masoko ya nje ya Tanzania.