KIKAO CHA KAMATI YA UKAGUZI, VIATARISHI NA FEDHA
Katika kikao Maalum cha Kamati ya Ukaguzi, Vihatarishi na Fedha, Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwaajili ya kupitia Rasimu ya Mahesabu kwa Mwaka wa fedha 2026/2027, wajumbe wa kamati hiyo wameitaka Menejimenti kubuni mikakati ya kibiashara itayowezesha kuongeza wigo wa biashara ya mbolea nchini.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo, tarehe Agosti 27, 2026, katika ukumbi wa Ofisi za TFC, Jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Boma Raballa ameeleza kuwa TFC kama Kampuni ya Serikali inafursa ya kukuza biashara ya mbolea, kuongeza wigo wa biashara ya mbolea na kuwafikia wakulima wa mazao yote ikiwemo zao la Miwa.
Katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, sekta ya kilimo imepewa kipaumbele katika kufikia malengo ya nchi ikiwemo kuwa na utoshelevu wa chakula, hivyo matumizi ya mbolea katika uzalishaji wa tija ni ya muhimu.
Pamoja na hayo wajumbe hao wameshauri juu ya kuwa na Mpango wa Biashara wa Kampuni ambao utakuwa dira ya uendeshaji wa biashara ili kuwafikia wakulima na wadau wengi zaidi katika kutoa huduma ya mbolea.

