RUVUMA WANUFAIKA NA MBOLEA YA RUZUKU
Wakulima na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kurahisisha upatikanaji wa mbolea ya ruzuku, hatua ambayo imeongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao.
Akizungumza kuhusu uwezeshwaji huo, Jackson Mapunda, ambaye ni mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo katika kata ya Lilambo, eneo la Likuyu Fusi, wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwasaidia wakulima kupata mbolea kwa njia ya ruzuku.
Aidha, ameishukuru kampuni ya TFC kwa kupeleka mbolea za kutosha katika eneo hilo, huku akiwahakikishia wakulima kuwa mbolea ipo ya kutosha na wanachotakiwa kuwa nacho ili kuipata ni namba zao za mkulima pekee.
Kwa upande wake, mmoja wa wakulima wa mahindi katika eneo hilo, Agusta Mapunda, ameeleza kuwa kabla ya kuanza kutumia mbolea za TFC, uzalishaji wake ulikuwa mdogo na hakuwa akipata mavuno ya kutosha, lakini kwa sasa, kutokana na matumizi ya mbolea hiyo, anafanikiwa kuvuna kuanzia roba 15 mpaka 20 kwa ekari moja.
Amesema kuwa ongezeko hilo la uzalishaji limemsaidia kupata faida
inayomwezesha kusomesha watoto, kupata chakula, na kukidhi mahitaji madogo madogo ya nyumbani.

