Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo aainisha fursa za Uwekezaji Katika Sekta ya Mbolea Tanzania
Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi (Tanzania–Russia Trade and Investment Forum) lililofanyika katika Ukumbi wa AICC jijini Arusha, limewakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili. Ambapo fursa za biashara na uwekezaji katika tasnia ya mbolea ni miongoni mwa sekta za kimkakati zilizojadiliwa kutokana na uhitaji mkubwa wa mbolea nchini.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema mbolea ni nyenzo muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini, hivyo kuna fursa kubwa za uwekezaji katika tasnia ya mbolea ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.
Katika mkutano huo, TFC imekutana na wadau wa mbolea na sekta ya kilimo za nchi ya Urusi na kujadiliana mikakati mbalimbali ya biashara na uwekezaji ikiwemo; Uagizaji wa mbolea za kutosha kutoka Urusi. Uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha na kuchakata mbolea kwenye maeneo ya kimkakati nchini Tanzania na kushirikiana na wataalam wa mbolea Urusi kwenye masuala ya utafiti na maendeleo ya mbolea.
Aidha, jukwaa hilo limeweka mkazo katika maeneo ya kilimo, madini, viwanda, nishati, teknolojia ya Habari na mawasiliano pamoja na elimu ya ufundi, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuongeza uzalishaji wenye tija.
Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imeshiriki katika mkutano huo uliojadili fursa za uwekezaji na biashara baina ya Urusi na Tanzania.

