Serikali Yaendelea Kuimarisha Sekta ya Mbolea kwa Kuzingatia Mifumo ya Kikanda na Bara
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Kilimo, inaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya mbolea kwa kukuza biashara na uwekezaji kupitia Mkutano wa ARGUS Africa Fertilizer Conference 2026 unaofanyika katika Jiji la Dar es Salaam.
Akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo, Naibu Katibu Mkuu (Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula), Prof. Peter Msofe, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa mbolea bora, salama na nafuu ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Fertilizer Company (TFC), Bw. Samuel Mshote alizungumza kwa niaba ya kampuni, akisisitiza jukumu lake la kusaidia wakulima kupata mbolea kwa wakati na kuunga mkono jitihada za Serikali za upatikanaji endelevu wa pembejeo za kilimo.
Juhudi hizi zinalingana na vipaumbele vya kikanda na Bara, ikiwemo Comprehensive Africa Agriculture Development Programme (CAADP), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na African Continental Free Trade Area (AfCFTA), kwa lengo la kuimarisha ushindani, biashara ya kikanda na upatikanaji endelevu wa pembejeo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, alisema matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 360,000 mwaka 2021/2022 hadi takribani tani milioni moja mwaka 2024/2025, na yanatarajiwa kufikia tani milioni 2.1 ifikapo 2030.

