CHONGOLO: KUWENI NA MABADILIKO YA FIKRA KUTAFUTA MATOKEO YENYE TIJA
Menejimenti ya Wizara ya Kilimo na Wakuu wa Taasisi zilizo chini yake wametakiwa kuwa na mabadiliko ya fıkra ili kuleta matokeo yenye tija kwa wakulima katika utekelezaji wa DIRA 2050, Ajenda 10/30 na Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Sekta ya Kilimo 2050.
Amesema hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), wakati akifungua Mafunzo Wezeshi kwa Wakuu wa Idara/Vitengo na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, yaliyofanyika tarehe 13 Julai 2026, jijini Arusha.
“Tuitumie nafasi tuliyopewa kwa uadilifu, uzalendo na kujituma. Tujenge taasisi zinazoheshimu sheria, zinazowajibika na zinazotoa huduma kwa viwango vya juu. Tuwe viongozi wanaosikiliza, wanaofanya maamuzi kwa wakati, wanaofuatilia utekelezaji na wanaowajibika kwa matokeo,” amesema Mhe. Chongolo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yamelenga kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha uwezo wa viongozi katika maeneo ya uongozi, usimamizi, mawasiliano, maadili na utoaji wa huduma bora, ili kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara na Serikali kwa ujumla.

