KIKAO CHA BODI YA WAKURUGENZI KUJADILI HALI YA UPATIKANAJI, UNUNUZI NA USAMBAZAJI WA MBOLEA KWA MSIMU WA KILIMO TFC 2026/2027
Bodi ya Wakurugenzi, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) wameitaka Menejiment kuhakikisha inakidhi mahitaji ya mbolea kwa wakulima kuelekea msimu wa kilimo ambapo Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TFC imepanga kununua na kusambaza kwa wakulima jumla ya tani 270,500 za mbolea.
Rai hiyo imetolewa Septemba 4, 2026 katika kikao maalumu kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za TFC, jijini Dar es salaam kujadili Taarifa ya Hali ya Upatikanaji, Ununuzi na Usambazaji wa Mbolea kwa msimu wa kilimo 2026/2027
Katika kikao hicho, Bodi ya Wakurugenzi wamesisitiza juu ya kuimarisha mahusiano na vyama vya Ushirika ili kupata fursa ya kusambaza mbolea kwa wakulima wa vyama hivyo.
Aidha, kama TFC ilivyofanikiwa kusambaza mbolea ya zao la tumbaku, Bodi ya Wakurugenzi wameitaka Menejiment kupitia vyama vya ushirika kuwafikia wakulima wa mazao mengine ikiwemo zao la Miwa na Pamba.
Kiasi cha tani 270,500 cha mbolea zitakazosambazwa kwa wakulima kinajumuisha tani 70,000 za mbolea ya kukuzia mazao (UREA), tani 65,000 za mbolea ya kupandia mazao (DAP), tani 10,000 za mbolea ya kuzalishia mazao (CAN), tani 5,000 za mbolea ya SA, tani 50,000 za mbolea kutoka kwa wazalishaji wa ndani, tani 500 za mbolea ya zao la Chai pamoja na tani 70,000 za mbolea za zao la tumbaku.
Hadi sasa TFC imeingiza nchini tani 33,000 za mbolea aina ya DAP, taratibu za kusambaza mbolea hizo katika vituo vya mauzo vilivyopo katika mikoa mbalimbali zinaendelea. Na jumla ya tani 2,459.75 za mbolea ya NPK kwaajili ya zao la tumbaku zimekabidhiwa kwa Umoja wa Vyama vya Ushirika vya Wakukima wa Tumbaku TCJE ili zisambazwe katika maeneo husika ya uzalishaji wa zao la hilo.

