Mkuu wa Mkoa wa Tabora Apongeza Uwekezaji wa Kiwanda Kikubwa cha Mbolea cha United Capital Fertilizer
Baada ya kukagua eneo hilo leo, Desemba 5, 2025, wawakilishi wa Kampuni ya United Capital Fertilizer wameeleza kuridhishwa kwao na hali ya mazingira ya eneo husika pamoja na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Mkoa katika kuratibu na kuwezesha utekelezaji wa mradi huo wa uwekezaji.
Kwa mujibu wa tathmini za awali, uwekezaji huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora na Tanzania kwa ujumla. Manufaa hayo yanajumuisha kuongezeka kwa ajira hususan kwa vijana, kuboresha upatikanaji wa mbolea kwa bei nafuu, pamoja na kuimarisha maendeleo ya kilimo cha kibiashara. Aidha, ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuongeza mapato ya mkoa na taifa kupitia kodi, sambamba na kuchochea mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa maeneo mengi nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paulo Chacha, amepongeza uamuzi wa Kampuni ya United Capital Fertilizer of Zambia kuwekeza nchini Tanzania kupitia ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea mkoani Tabora, akibainisha kuwa uwekezaji huo utaongeza tija kwa wakulima wa ndani na nje ya mkoa huo.
Mheshimiwa Chacha ameeleza hayo wakati wa ziara ya kutathmini fursa za uwekezaji, ambapo alitembelea eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho lililopo Kata ya Ilolangulu, Wilaya ya Uyui. Eneo hilo lina ukubwa wa zaidi ya ekari 2,000 na limependekezwa kutokana na sifa zake za kimkakati pamoja na upatikanaji wa ardhi unaokidhi mahitaji ya shughuli za viwanda.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Apongeza Uwekezaji wa Kiwanda Kikubwa cha Mbolea cha United Capital Fertilizer

