Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Kampuni ya Mbolea Tanzania

UTAFITI WA AFYA YA UDONGO NI MUHIMU KWANI UNATUWEZA KUELEWA NI AINA GANI YA MBOLEA INAYOPASWA KUTUMIWA KATIKA KILIMO.

Imewekwa: 08 Jul, 2025
UTAFITI WA AFYA YA UDONGO NI MUHIMU KWANI UNATUWEZA KUELEWA NI AINA GANI YA MBOLEA INAYOPASWA KUTUMIWA KATIKA KILIMO.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) Ndg. Samuel Mshote ameeleza kuwa utafiti wa afya ya udongo ni muhimu kwani unawezesha kufahamu ni aina gani ya mbolea itumike katika kilimo.

Ameyasema hayo leo tarehe 06.07.2025 alipotembelea katika banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. J. K Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar es salaam alipotembelea kuona shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo ikiwemo upimaji wa afya ya udongo.

“Tunapoelekea kuanza kuzalisha mbolea ya ruzuku ndani ya Nchi, ni wakati muafaka wa kushirikiana na TARI ili kuzalisha mbolea inayoendana na afya ya udongo ya sehemu husika,” ameeleza Ndg. Mshote

Sambamba na hayo ameeleza kuwa ufungaji  mtambo wa kuchanganya mbolea (Blending Fertilizer Facility) wenye uwezo wa kuchanganya tani 120 kwa saa upo katika hatua ya ukamilishaji.

Pamoja na hayo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ametembelea banda la Wizara ya Kilimo na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo, ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Wakala wa Mbegu (ASA), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC).