Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Kampuni ya Mbolea Tanzania

Skimu za Umwagiliaji na Ruzuku ya Mbolea kuwanufaisha wakulima wengi zaidi nchini

Imewekwa: 24 Feb, 2024
Skimu za Umwagiliaji na Ruzuku ya Mbolea kuwanufaisha wakulima wengi zaidi nchini

Sekta ya Kilimo inaendelea kuimarika kikamilifu kutokana na uboreshaji unaoendelea kwenye Kilimo cha Umwagiliaji pamoja na matumizi ya Ruzuku ya Mbolea.

Kwa sasa Wizara ya Kilimo inaendelea kuchukua hatua kadhaa katika kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Mabwawa ya Umwagiliaji huku ikikabiliana na kasoro zilizojitokeza kwenye usambazwaji wa ruzuku ya mbolea kwenye msimu uliopita.

Hatua zinazochukuliwa na serikali zenye lengo la kuboresha Miundombinu ya Umwagiliaji  na matumizi ya mbolea zimefafanuliwa zaidi na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) leo Februari 14  2024 wakati akijibu baadhi ya maswali ya wabunge waliokuwa wakitaka kupatiwa ufafanuzi kuhusiana na masuala mbalimbali yahusuyo Skimu za Umwagiliaji na Ruzuku ya Mbolea.

Akijibu swali la Mhe. Hassan Zidadu Kungu (Mbunge wa Tunduru Kaskazini) aliyetaka kufahamu lini ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Kijiji cha Nambalapi Kata ya Masonya – Tunduru utaanza, Naibu Waziri Silinde amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika skimu ya Nambalapi yenye ukubwa wa Hekta 300.

“Ujenzi wa skimu hii, umeingizwa kwenye mpango bajeti katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo taratibu za manunuzi za kumpata mkandarasi atakayejenga miundombinu ya umwagiliaji zinaendelea, baada ya kukamilisha hatua za manunuzi ujenzi wa skimu utaanza mara moja”, amesema Mhe. Silinde.

Ameongeza kwa kusema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa skimu hiyo utanufaisha zaidi ya wakulima 5,933 katika vijiji vya Masonya, Nakayaya Mashariki, Mkalekawana, Nambalapi na maeneo jirani ndani ya Wilaya ya Tunduru.

Mhe. Silinde akijibu swali la Mhe. Anna Richard Lupembe (Mbunge wa Nsimbo) aliyetaka kufahamu lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa Umwagiliaji katika Kata ya Urulwa Kijiji cha Usense – Nsimbo, Mhe. Silinde amesema kuwa ujenzi wa mradi wa umwagiliaji wa Usense ulianza mwaka wa fedha 2021/2022 na ujenzi huu ulikusudiwa kukamilika baada ya miezi sita. Hata hivyo, ujenzi wa miundombinu katika skimu hii haukukamilika kutokana na mkandarasi kushindwa kutekeleza kazi kulingana na mkataba hali iliyopelekea mkataba kusitishwa.

“Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetangaza upya zabuni ya mradi huo ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Usense. Mchakato wa manunuzi utakapokamilika, ujenzi utaanza mwara moja. Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wakazi wa vijiji vya Usense, Urulwa na Ikondamoyo,” ameeleza Mhe. Silinde.