Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Kampuni ya Mbolea Tanzania

Neema zaidi kwa wakulima nchini yaja

Imewekwa: 24 Feb, 2024
Neema zaidi kwa wakulima nchini yaja

Katika kuhakikisha wakulima nchini wananufaika na mbolea za ruzuku, Wizara ya Kilimo imeziagiza kampuni za mbolea kuhakikisha zinafunga mbolea hiyo kwenye vifungashio vya kilo tano, 10, 20, 25, 30 na 50.

Hatua hii inaenda kuwakomboa wakulima ambao awali walikuwa wakilazimika kununua mbolea ya kilo 50.

Akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph Kakunda aliyetaka kufahamu ni lini mbolea ya ruzuku itaanza kuuzwa kwa bei elekezi inayozingatia ujazo wake, Waziri Bashe amesema kwa sasa mbolea ya ruzuku imeshaanza kusambazwa na kutoa agizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha kampuni za uuzaji wa mbolea zinafungasha mbolea kwa ujazo wa kilo tano, 10, 20 na kilo 50.

“Ninaagiza TFRA popote mlipo hakikisheni kuwa kunakuwa na vifungashio vya ujazo tofauti tofauti kuanzia kilo tano, 10, 20 na 50 na hakikisheni kuwa hata kwa wale wanaofunga kwa kilo labda iwe tano tano ikafika hata mifuko 10 yani ikawa kilo 50 bado bei yake ya uuzwaji haitakiwi kuzidisha thamani ya bei elekezi ya shilingi elfu sabini na tano kwa kilo 50,” amesema Waziri Bashe.

Ametumia pia wasaha huo kuziagiza kampuni za mbolea kuzingatia masharti ya uuzaji na kuepuka kuzidisha kiwango cha bei elekezi huku akitolea mfano wa kampuni iliyofungasha ujazo wa mifuko kumi ya kilo tano tano na kupata jumla ya kilo 50 ambapo iliuza mifuko hiyo ya kilo tano tano kwa Shilingi 13,000 kwa mfuko, hivyo kujikuta ikipata Shilingi 130,000.

Kuhusiana na changamoto ya wakulima wa Tumbaku kukosa bei ya Pembejeo mwaka 2023, Waziri Bashe amejibu kuwa kwa sasa Serikali inafanya kikokotoo kuona ni namna gani wakulima wa tumbaku wanapata ruzuku ya pembejeo na kuwahakikishia kuwa watanufaika na pembejeo kupitia mjumuiko wao wa wakulima wa Tumbaku.

Pia Waziri Bashe alijibu swali la Mbunge wa Kisesa- Mwanza, Mhe. Luaga Mpina aliyetaka kufahamu ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto za ugawaji wa ruzuku ya mbolea zilizojitokeza kwa msimu uliopita ambapo Waziri Bashe alieleza kuwa Serikali imezichukua changamoto hizo kujipanga katika kuhakikisha kuwa msimu huu hazijirudii katika utoaji wa ruzuku hiyo ya mbolea.

“Nakiri kuwa kwa msimu uliopita kulikuwa na changamoto kadhaa lakini kwa msimu huu changamoto kubwa ni kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaotaka kutorosha mbolea kwenda nje ya nchi kwa kuwa wameshindwa kuiba kwenye mfumo, wameshindwa kuiba kwa kutoa takwimu hewa kwa kuwa huko kote tumebana, kwa sasa wanataka kutorosha kwenda nje ya nchi,” ameeleza Waziri Bashe. 

Ameongeza kuwa “Mikoa ya Songwe na Kigoma wapo wafanyabiashara ambao wameshakamatwa na kupandishwa mahakamani kwa makosa hayo na kushtakiwa kwa uhujumu uchumi na niwahakikishie wakulima kuwa Serikali inazidi kuboresha mfumo ili mhudumiwe vema zaidi.”