Accessibility Settings

Text Size

Color Contrast

Language

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Kampuni ya Mbolea Tanzania

/ News

ELIMU YA MBOLEA YABADILI MTAZAMO WA WAKULIMA MEATU

Imewekwa: 13 December, 2025
ELIMU YA MBOLEA YABADILI MTAZAMO WA WAKULIMA MEATU

Wakulima wa Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu, wamebadili mtazamo wao kuhusu mbolea kuwa ni chanzo cha uharibifu wa udongo, ambapo sasa wamepata elimu kuwa matumizi ya mbolea ni nyenzo muhimu ya kuuwezesha udongo kurudisha uhai wake na kuchochea uzalishaji wa mazao.

Haya yamebainishwa wakati wa mafunzo waliyopatiwa na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na taasisi zake tarehe 04 Desemba 2025 mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bi. Newaho Mkisi, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo, hususan mbolea na mbegu.

Bi. Mkisi amesema kuwa mahitaji ya mbolea Wilayani humo yameongezeka sana tofauti na ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita. Ameeleza kuwa kwa sasa wakulima wanaelewa kuwa mbolea siyo adui wa udongo bali ni kirutubisho muhimu katika ukuaji wa mmea.

Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Godwin Vedastus, ameeleza kuwa mbolea haiharibu udongo. Kinyume chake, mbolea inauongezea udongo virutubisho ambavyo mimea inahitaji ili kustawi kwa afya na uzalishaji wenye tija.